KLABU za Simba na Yanga jana ziliwekwa kiti moto na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhusu uharibifu wa miundombinu uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mechi iliyoikutanisha miamba hiyo ya soka mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Uwanja wa Taifa ambapo kilijumuisha viongozi wa Simba, Yanga, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara kupitia Mkurugenzi wa Michezo, Makoye Nkenyenge.
Hatua hiyo ya Wizara imekuja siku moja baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kutangaza kuzifungia timu hizo kutumia Uwanja wa Taifa kutokana na mashabiki wake kuvunja viti 1781 na milango miwili ya kuingilia uwanjani, katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Aidha, Nape alizuia mapato ya mechi hiyo mpaka tathmini kamili itakapofanyika kujua gharama za vitu vilivyoharibiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara hiyo, Makoye Nkenyenge ambaye aliitisha kikao hicho, alisema aliwaita wadau hao katika kikao chao cha siri kwa ajili ya kutathmini uharibifu huo na kujipanga kutoa elimu ya utunzwaji miundombinu kwa mashabiki.
“Ilikuwa ni kikao chetu cha siri, lakini lengo letu lilikuwa kutathmini uharibifu na kujipanga namna ya kuelimisha wadau jinsi ya kutunza miundombinu,”alisema.
“Lakini hatukuwaalika vyombo vya habari kwa kuwa yalikuwa mambo yetu”.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit na Katibu wa TFF Selestin Mwesigwa walikiri kukutana jana lakini walisema kilichojadiliwa kitazungumzwa na Wizara.
No comments:
Post a Comment